Rais Ruto azuru kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote nchini Nigeria

Ziara hiyo ya Rais Ruto inajiri, huku akitarajiwa kuzindua ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote East Africa, kaunti ya Lamu juma lijalo.

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais Ruto azuru kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote nchini Nigeria.

Rais William Ruto amezuru kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote katika jimbo la Lekki, nchini Nigeria, kwa mwaliko wa Rais wa kampuni hiyo, Aliko Dangote.

Ziara hiyo ya Rais Ruto inajiri, huku akitarajiwa kuzindua ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote East Africa, katika kaunti ya Lamu juma lijalo.

Kiwanda hicho nchini Nigeria husafisha takriban mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku, na kuzalisha zaidi ya lita milioni 100 ya petroli, diesel na mafuta ya ndege kila siku.

Kampuni hiyo imejenga kilomita 120 ya mabomba  baharini kwa usafirishaji wa mafuta kutoka kwa meli hadi kiwanda hicho.

Kiwanda cha Kusafisha mafuta cha Dangote nchini Nigeria.

Kwenye ziara hiyo, Rais Ruto alisema ufanisi wa kiwanda hicho cha Dangote nchini Nigeria, ni ishara ya yale yanaweza afikiwa na serikali za Afrika, wawekezaji na taasisi za kifedha iwapo zitashirikiana pamoja.

“Ujenzi ambao tutauzindua nchini Kenya juma lijalo utakuwa mkubwa. Utabadilisha sekta ya petroli nchini Kenya na kanda nzima kwa jumla na kuhakikisha usalama wa mafuta, pamoja na kubuni nafasi 60,000 za ajira,” alisema Rais Ruto.

Aliongeza kuwa ujenzi huo utakapokamilika, viwanda kadhaa vitazinduliwa ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa mbolea, kemikali na upakiaji.

Share This Article