Maandamano yameibuka nchini Msumbiji dhidi ya chama tawala Frelimo baada ya kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi ulioghubikwa na utata wa mwezi jana.
Maafisa wa polisi walilazimika kutumia vitoza machozi kutawanya waandamanaji waliojitokeza kufuatia hasira ambayo imekuwa ikiongezeka tangu Frelimo kutajwa mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 9, 2024 na kuendeleza utawala wake wa miaka 49.
Mashirika ya kutetea haki za binaamu yanaripoti vifo 18 vilivyotokea kwenye makabiliano kati ya polisi na waandamanaji tangu ushindi wa Frelimo ulipotangazwa.
Uchaguzi huo mkuu ulishuhudia ushindani mkali ambapo watu wengi wa umri mdogo walikuwa wanamuunga mkono mwaniaji huru wa urais Venancio Mondlane, aliyeitisha maandamano akisema ulikumbwa na visa vya udanganyifu.
Maandamano aliyoitisha Mondlane ni ya wiki nzima na Alhamisi Novemba 7, 2024 ndio yalichacha zaidi.
Waangalizi wa uchaguzi huo kutoka mataifa ya magharibi na watetezi wa haki pia walikubali kwamba matokeo ya uchaguzi yalibadilishwa.
Mondlane wa umri wa miaka 50 aliyekuwa mtangazaji wa redio anahisi kwamba huu ni wakati muhimu kwa nchi ya Msumbiji.
“Ninahisi kwamba kuna mazingira ya mapinduzi, ishara kwamba tuko ukingoni mwa mabadiliko ya kipekee ya kihistoria nchini humu.” alisema Mondlane ambaye hajafichua aliko ila amesema hayuko barani Afrika.
Muungano wa mawakili nchini Msumbiji – Mozambique Bar Association – umeonya kwamba mazingira yaliyoko nchini humo sasa ni ya mauaji ya wengi.
Jana Alhamisi jiji kuu la Maputo, ambalo ni makazi ya zaidi ya watu milioni moja, lilisalia mahame huku maduka, benki, taasisi za elimu na maeneo mengine muhimu yakiwa yamefungwa.
Matumizi ya mtandao yamebanwa huku kamishna wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Volker Turk, naye akionya dhidi ya nguvu kupita kiasi kwenye makabiliano.
Anahisi kwamba maafisa wa polisi wanafaa kusimamia maandamano kulingana na wajibu wa kimataifa wa msumbiji wa haki za binadamu.