Rais William Ruto amewasili jijini Addis Ababa nchini Ethiopia ambako atahudhuria kikao cha Kawaida cha 38 cha Baraza la Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).
Ruto amesema anatazamia mazungumzo yatakayofanywa kuhusiana na juhudi zinazoendelea za kuifanyia AU marekebisho.
“Natazamia mzungumzo juu ya marekebisho ya Umoja wa Afrika na uchaguzi wa Tume ya Umoja wa Afrika, ambayo Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga anatafuta kuwa mwenyekiti wake.”
Ruto amekuwa mstari wa mbele kumpigia debe Raila kumrithi Moussa Faki ambaye muda wake wa kuhudumu unakamilika baada ya kuhudumu kwa mihula miwili.
Wakati akiwa Addis Ababa, Ruto anatazamiwa kumnadi Raila kwa viongozi wengine wa Afrika kabla ya upigaji kura kufanyika keshokutwa Jumamosi.
Raila atamenyana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Madagascar Richard Randriamandrato.
Mgombea huyo wa Kenya ameelezea matumaini kuwa atautwaa wadhifa huo hasa baada ya kufanya kampeni kali ambapo alitembelea mataifa mbalimbali ya Afrika kujinadi kwa viongozi wa nchi hizo.
Jana Jumatano, Raila alikuwa mjini Bujumbura kutafuta uungwaji mkono kabla ya kuelekea Addis Ababa.