Seneta wa Samburu Lelegwe Ltumbesi, ametoa wito wa uchunguzi kufanywa kuhusu madai ya mauaji ya mifugo na kupigwa risasi kwa wakazi wakati wa operesheni ya kiusalama katika wakilishi wadi ya Waso, eneo bunge la Samburu ya Mashariki.
Ltumbesi aliambia Bunge la Senate kuwa mbuzi 415 na ng’ombe 102, waliuawa na maafisa wa usalama katika muda wa siku tatu, ambapo wakazi pia walipata majeraha ya risasi.
Kulingana na Seneta huyo, maafisa wanaodaiwa kuhusika ni wale wa General Service Unit (GSU) na maafisa wa kitengo cha kukabiliana na wezi wa mifugo (ASTU).
“Siku ya Jumamosi, maafisa waliwapiga risasi na kuwaua mbuzi 15 wanaomilikiwa na jamii ya Lekilwai, na ng’ombe wawili katika eneo la Losesia,” alisema Seneta huyo.
Kulingana na Seneta huyo, hali iliendelea kuwa mbaya zaidi siku mbili baadaye, wakati mamia ya mifugo wlipouawa.
“Siku ya Jumatatu maafisa hao waliwaua mbuzi 400 wanaomilikiwa na familia ya Lekalantula na ndama 100, wanaomilikiwa na familia za Lesurmaat, Laigwanani na Lolpuranai katika eneo la Nolng’erdeed,” alidokeza Ltumbesi.
Aidha, alifahamisha Bunge la Senate kuwa siku hiyo hiyo, Leapem na Lesidiya walipigwa risasi na kujeruhiwa katika maeneo ya Nolng’erdeed na Losesia mtawalia.
Alihoji matokeo ya operesheni hiyo ya kiusalama, akisema hakuna mshukiwa yeyote wa ujangili alikamatwa au kupatikana kwa mifugo walioripotiwa kuibwa.
Seneta huyo alitoa wito wa uchunguzi wa kina kufanywa na Halmashauri ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA) na kitengo cha maswala ya ndani (IAU).
Vikao vya Bunge la Senate vinaandaliwa katika kaunti ya Kilifi, kwenye mpango wa kila mwaka wa Senate Mashinani.