Maafisa wa Polisi kaunti ya Kiambu wanamtafuta mshukiwa anayedaiwa kuwaua wafanyakazi wenza wawili, na kumjeruhi mmoja vibaya katika mtaa wa Mugumo Drive Kiambu mjini.
Mshukiwa huyo Moses Kigera, alitoroka eneo la mkasa baada ya kutekeleza mashambulizi hayo.
Kulingana na afisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai kaunti ndogo ya Kiambu Mashariki Stephen Mutua, polisi walifahamishwa na mmoja wa wafanyakazi aliyetoroka kuhusu mashambulizi hayo, na walipofika kwenye eneo la tukio walipata miili ya wawili hao pamoja na silaha zinazoaminika zilitumika.
Polisi walisema chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana, lakini Kamanda wa Polisi eneo la Kiambu Mashariki Elema Hassan, alisema uchunguzi wa awali uliashiria kuwa mshukiwa huyo aliachishwa kazi hivi karibuni na nafasi yake kuchukuliwa na mmoja wa waathiriwa.
Maafisa wa polisi wamesema uchunguzi unaendelea kuhusiana na mauaji hayo, huku msako dhidi ya mshukiwa ukianzishwa.
Miili hiyo miwili inahifadhiwa katika chumba cha maiti katika hospitali ya Kiambu Level 5, huku aliyejeruhiwa akipokea matibabu katika hospitali hiyo.