Hakimu, afisa wa urekebishaji tabia wakamatwa kwa madai ya ufisadi

Tom Mathinji
1 Min Read
Hakimu, afisa wa urekebishaji tabia wakamatwa kwa madai ya ufisadi.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), imemkamata Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama ya Kangema pamoja na Afisa Mkuu wa Urekebishaji Tabia, kwa madai ya kushiriki ufisadi ili kuvuruga matokeo ya kesi ya uhalifu.

Washukiwa hao Martin Kinyua Mutegi, ambaye ni Hakimu Mkuu na Julius Irungu Njogu, Afisa Mkuu wa Urekebishaji Tabia, walikamatwa Jumanne Julai 21, 2026 katika hoteli moja Kangema Mjini baada ya tume hiyo kutekeleza operesheni.

Operesheni hiyo ilitekelezwa baada ya mfanyabiashara wa Kaunti ya Murang’a kuripoti kuwa alishtakiwa Julai 2, 2026 katika kesi ya uhalifu kwa kupokea pesa kwa njia ya ulaghai na kwamba alitarajiwa kuhukumiwa Julai 22, 2026.

Uchunguzi wa awali ulibainisha kuwa afisa huyo wa urekebishaji tabia alidai kuwa ametumwa na Hakimu huyo Mkuu kumtaka mfanyabiashara huyo atoe shilingi 170,000, ili asihukumiwe.

EACC ilianzisha  operesheni na kuwakamata wawili hao wakipokea shilingi 150,000 kutoka kwa mlalamishi huyo.

Wanazuiliwa katika kituo cha polisi  cha Central Nyeri mjini wakisubiri hatua zaidi za kisheria dhidi yao.

TAGGED:
Share This Article