Merino aipeleka Uhispania nusu fainali ya Kombe la Dunia

Nusu fainali ya kwanza itasakatwa Jumanne ijayo Julai 14 ,Uhispania wakiwa na miadi dhidi ya Ufaransa.

Dismas Otuke
1 Min Read

Nguvu mpya Mikel Merino, alipachika bao la dakika ya 88 na kuisaidia Uhispania, kuinyuka Ubelgiji mabao 2-1, na kufuzu kwa nusu fainali ya Kombe la Dunia Ijumaa usiku katika uwanja wa Los Angeles,nchini Marekani.

Uhispania walitangulia kufunga bao kunako dakika ya 30 kupitia kwa Fabian Ruiz, lakini Charles De Ketelare,  akakomboa kwa Ubelgiji,dakika 11 baadaye na kipindi cha kwanza kumalizikia sare ya 1-1.

Kipindi cha pili timu zote zilijihami huku zikitumia mashambulizi ya kushtukiza bila mafanikio.

Hata hivyo ,Red Devils ya Ubelgiji, walipatwa na pigo baada ya kipa Thibaut Courtois, kujeruhiwa na kuondolewa uwanjani dakika ya 71.

Zikisalia dakika mbili kipenga cha mwisho kipulizwe kipa nguvu mpya wa Ubelgiji Senne Lammens, alipangua mkwaju wa Pau Cubarsi, na ukampata Merino aliyeutuliza kimiani kwa bao la ushindi.

Uhispania watakuwa wakicheza nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010, walipotawazwa mabingwa.

Nusu fainali ya kwanza itasakatwa Jumanne ijayo Julai 14 ,Uhispania wakiwa na miadi dhidi ya Ufaransa.

Share This Article