Kamati ya Seneti ya Fedha na Bajeti imeipa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma, PPRA siku saba kuhakiki rekodi za ununuzi za kaunti ya Homa Bay na kuwasilisha ripoti ya mwisho.
Agizo hilo lilitolewa baada ya kikao cha leo Alhamisi, Oktoba 1, 2026 cha kamati hiyo na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga kuhusu masuala ya uzingatiaji wa sheria za ununuzi yaliyowasilishwa na mamlaka hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati, Seneta Ali Roba, aliagiza PPRA kulinganisha nyaraka zilizowasilishwa na kaunti na rekodi zilizopakiwa kwenye Tovuti ya Taarifa za Ununuzi wa Umma, PPIP kabla ya Seneti kuchukua hatua zaidi.
“Hatutakubali taarifa hizo kama zilivyo bila kuhakikiwa,” Roba alisema, akisisitiza umuhimu wa uhakiki huru wa rekodi hizo.
Maafisa wa Homa Bay waliiambia kamati kuwa nyaraka za ununuzi pamoja na ripoti za Fursa za Ununuzi wa Serikali kwa Makundi Maalum, AGPO, zilikuwa zimepakiwa kwenye mfumo huo.
Gavana Wanga alisisitiza kujitolea kwa kaunti katika uwazi, uwajibikaji na uzingatiaji wa sheria za ununuzi.
Seneta Tabitha Mutinda alisema baadhi ya changamoto zilionekana kusababishwa na ucheleweshaji wa kiutawala na mawasiliano kati ya maafisa wa kaunti na PPRA.
Wanga pia alielezea kesi ya mahakamani inayoendelea kuhusu malipo ambayo hayajakamilika chini ya mkataba wa kaunti, akisema suala hilo lilipitia mchakato mrefu wa ukaguzi na upatanisho.