Seneti yaalika maoni ya umma kuhusu mswada wa Dhahabu

Maoni hayo ni lazima yamfikie Karani wa Seneti mnamo au kabla ya Jumatano, Oktoba 7, 2026, saa 11:00 jioni.

Marion Bosire
2 Min Read
Amason Kingi - Spika wa Bunge la Seneti

Bunge la Seneti limealika umma rasmi kuwasilisha maoni kuhusu Mswada wa Usindikaji wa Dhahabu wa mwaka 2023.

Mswada huo ni pendekezo la kisheria linalokusudiwa kuanzisha mfumo huru wa udhibiti kwa sekta ya usafishaji wa dhahabu nchini Kenya.

Mswada huo wa Bunge la Kitaifa Nambari 46 wa mwaka 2023, uliosomwa kwa mara ya kwanza Septemba 8, 2026, kwa sasa unakaguliwa na Kamati ya Kudumu ya Seneti kuhusu Ardhi, Mazingira na Maliasili.

Sheria hiyo inayopendekezwa inalenga kutenganisha masuala ya usindikaji wa dhahabu kutoka kwenye Sheria kuu ya Madini katika Sura ya 306.

Itaunda chombo maalumu na cha kati kitakachopewa jukumu la kusimamia viwango vya kitaifa, kupata ithibati ya kimataifa na kufuatilia viwanda vya usafishaji pamoja na maabara.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 118 cha Katiba, kamati hiyo inahakikisha ushiriki wa umma unakuwepo kabla ya kuwasilisha ripoti yake ya mwisho.

Wananchi na wadau wanahimizwa kuwasilisha maoni yaliyoandikwa yanayoainisha mapendekezo yao, na ni lazima mawasilisho hayo yamfikie Karani wa Seneti mnamo au kabla ya Jumatano, Oktoba 7, 2026, saa 11:00 jioni.

Maoni yanaweza pia kuwasilishwa moja kwa moja katika Majengo Makuu ya Bunge jijini Nairobi, kutumwa kwa njia ya posta, au kutumwa moja kwa moja kwa barua pepe kwa karani wa Seneti na kamati husika.

Mswada mzima na muhtasari wake vinapatikana kwenye tovuti rasmi ya Bunge.

Share This Article