Kindiki aahidi uchaguzi ujao utakuwa huru na wa haki

Martin Mwanje
2 Min Read
Naibu Rais prof. Kithure Kindiki akiwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi kwenye Kongamano la Ushirikiano wa Maendeleo Septemba 16, 2026

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki ametoa hakikisho kwa Wakenya na washirika wa maendeleo kwamba uchaguzi mkuu ujao utakuwa huru, wa haki na wa kuaminika.

Akizungumza leo Jumatano wakati wa Kongamano la 15 la Ushirikiano wa Maendeleo mtaani Karen jijini Nairobi, Prof. Kindiki amefutilia mbali hofu kuwa uchaguzi huo utaghubikwa na hata chembe moja ya udanganyifu wala vurugu.

Hakikisho lake linakuja wakati ambapo madai ya Katibu Mkuu wa chama cha UDA Hassan Omar kwamba hata wafu watapiga kura kwenye uchaguzi huo yameibua mdahalo mzito nchini.

Wengi wakichambua kauli hizo kuwa njama ya chama tawala cha UDA kutaka kuiba kura wakati wa uchaguzi huo ili kusalia madarakani.

Hassan amekanusha kuwahi kusema chama cha UDA kitatumia wafu kupiga kura akidai alinukuliwa visivyo.

Badala yake, amesema alichomaanisha ni kwamba watu “waamke na wajitokeze kupiga kura.”

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) pia imewahakikishia Wakenya kwamba uchaguzi ujao utakuwa huru na wa haki, ikpuuzilia mbali madai ya kutumiwa kwa wafu kupiga kura kwenye uchaguzi huo.

Wakati huohuo, Kindiki ametoa hakikisho la utendaji kazi huru wa vyombo vya habari na mashirika ya kijamii nchini.

Kumekuwa na visa vya wanahabari kushambuliwa kwenye mikutano ya kisiasa na hata baadhi kutekwa nyara, hali ambayo imeibua mashaka miongoni mwa wadau kuhusu hatima ya uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Baadhi ya mashirika ya kijamii pia yamelalamikia kuminywa kwa uhuru wao.

 

 

Share This Article