Serikali yawekeza shilingi bilioni 39 kwa ujenzi wa barabara Meru

Kindiki alisema serikali imetoa rasilimali za kutosha, akielezea imani kwamba mwanakandarasi atakamilisha ujenzi huo kwa wakati.

Tom Mathinji
1 Min Read
Naibu Rais Kithure Kindiki akagua ujenzi wa barabara kaunti ya Meru.

Naibu Rais Kithure Kindiki ametangaza kuwa serikali imewekeza shilingi bilioni 39 zitakazotumika katika ujenzi wa barabara katika kaunti ya Meru.

Kindiki alisema barabara kadhaa ambazo wakazi wamekuwa wakisubiri kwa miaka kadhaa, sasa zinajengwa na ziko katika viwango tofauti vya ujenzi ikiwa ni pamoja na barabara ya Kionyo-Kanyakine-Muti O’Kiama-Ketha Kanaro-Mitunguu.

Akizunguma katika eneo la Imenti Kusini, Kindiki alisema serikali imetoa rasilimali za kutosha, akielezea imani kwamba mwanakandarasi atakamilisha ujenzi huo kwa wakati.

“Tumesubiri ujenzi wa barabara hii kwa muda mrefu. nimeona kwamba ujenzi wake unaendelea vyema. Mwanakandarasi huyu atakamilisha barabara hii,” alisema Kindiki.

Kulingana na Kindiki, serikali itashughulikia mahitaji ya miundombinu ya taifa hili, huku miradi hiyo ikitekelezwa kuambatana na rasilimali zilizopo.

“Tutajenga barabara zote moja baada ya ingine, hatua kwa hatua. Roma haikujengwa kwa siku moja,” alisema Kindiki.

Share This Article