Shirika la Utangazaji Nchini Kenya, KBC linaomboleza kifo cha mfanyakazi wa Radio Taifa, Edmonds Kweyu Salasya, aliyefariki dunia baada ya kuugua akiwa nyumbani.
Katika taarifa ya ndani ya shirika iliyotolewa Septemba 10, 2026, Mkurugenzi Mkuu na Afisa Mkuu Mtendaji wa KBC, Bi. Agnes Kalekye Nguna, alitoa pole kwa wafanyakazi na familia ya Salasya kufuatia kifo chake cha ghafla.
Salasya alikuwa akihudumu kama Mtayarishaji Msaidizi wa vipindi katika idara ya redio ambako wenzake wamemtaja kuwa mtaalamu aliyejitolea, anayeaminika na mfanyakazi aliyekuwa na mchango muhimu katika studio za shirika hili.
Alikuwa anaongoza kipindi cha Redio Taifa kiitwacho Usiku Mwema kilichokuwa kikipeperushwa saa mbili hadi saa 6 usiku.
“Shauku yake katika kazi na mchango wake kwa Shirika utamkumbukwa sana,” Nguna alisema katika taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, KBC ilipokea taarifa za kuugua kwa Salasya asubuhi ya Septemba 10. Alikimbizwa hospitalini kwa matibabu ya haraka, lakini alifariki dunia licha ya juhudi za wahudumu wa afya kuokoa maisha yake.
Mwili wake umepelekwa katika makafani ya Montenzuma na taarifa zaidi zitatolewa baada ya kuthibitishwa na familia.
Uongozi wa KBC pia umetangaza mipango ya kutoa ushauri nasaha wa kitaalamu kwa wafanyakazi walioathiriwa na msiba huo.
Nguna amewataka wafanyakazi kusaidiana wanapomlilia mwenzao na kuiweka familia ya Salasya katika mawazo na maombi yao.
“Mungu ailaze roho yake mahali pema penye wema.”