Mfanyabiashara ashtakiwa kwa ulaghai wa shilingi milioni 15 Nairobi

Martin Mwanje
1 Min Read

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) amemshtaki mfanyabiashara Walter Wekhanya Keya kwa mashtaka matatu yanayohusiana na madai ya ulaghai wa shilingi milioni 15.1. 

Anakabiliwa na mashtaka ya kupanga njama ya kulaghai, kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu na kuwa na fedha za uhalifu.

Keya alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi Stephany Bett katika mahakama ya Makadara ambapo alikanusha mashtaka dhidi yake.

Mahakama iliambiwa kwamba kati ya mwezi Mei na Oktoba mwaka 2023 huko Drive Inn, kaunti ndogo ya Starehe jijini Nairobi, Keya pamoja na wengine walipanga njama  ya kujipatia shilingi milioni 15.1 kutoka kwa Constant Wanyonyi kwa kusingizia kuwa wangeziwekeza katika biashara.

Katika shtaka la pili, Keya anadaiwa kupata shilingi milioni 5.1 kutoka kwa Wanyonyi, akiwa na wenzake, kupitia ulaghai.

Shtaka la tatu linaelezea kuwa Keya alikuwa na shilingi milioni 5.1 akifahamu vema kuwa zilipatikana au zilikuwa sehemu ya uhalifu uliofanywa naye na wenzake.

Keya aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 10 na mdhamini wa kiasi kama hicho, au dhamana mbadala ya shilingi milioni 5 pesa taslimu baada ya upande wa mashtaka kutopinga kuachiliwa kwake kwa dhamana.

Share This Article