Serikali za kaunti zimehimizwa kufuta leseni zote za baa na maeneo yanayouza pombe haramu katika vijiji, mojawapo ya hatua zinazolenga kukabiliana na kuenea kwa pombe hatari.
Mbunge wa Manyatta, Gitonga Mukunji, pia amezitaka serikali za ugatuzi kuchapisha hali ya leseni za vituo vyote vilivyosajiliwa vya uuzaji wa pombe vilivyoko katika kila wadi nchini.
Mukunji, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha wabunge wa umri mdogo, yaani Young Parliamentarian Association, alisema pombe haramu inaangamiza vijana, ambao ndio nguzo ya maendeleo na mustakabali wa Kenya.
Anataka wizara ya usalama wa ndani na utawala wa kitaifa kuongeza haraka operesheni za kukabiliana na maeneo ya utengenezaji wa pombe haramu katika kila kaunti, kwa ushirikiano wa karibu na wasimamizi wa kaunti, machifu na huduma ya taifa ya polisi.
“Wizara inapaswa kupeleka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI kufuatilia na kuvunja mitandao ya ufadhili na magenge yanayohusika na uzalishaji na usambazaji wa pombe haramu, badala ya kuwafuatilia wazalishaji wadogo pekee huku wafadhili wakubwa wakiendelea kubaki bila kuguswa,” alisema.
Himizo la Mukunji linajiri wakati ambapo wasiwasi umeshuhudiwa kati ya wanaotumia vileo nchini baada ya utafiti wa kampuni ya Euromonitor International, kuonyesha kwamba asilimia 60 ya vileo vyote vinavyouzwa nchini Kenya ni haramu, bandia au visivyoafiki viwango.
Ripoti ya utafiti huo iliyozinduliwa na Chama cha Vinywaji vya Vileo nchini Kenya, ABAK imesababisha hofu kote nchini huku viongozi wakitafuta suluhisho.