Rais William Ruto amewaaga Mabalozi wa Ufaransa na Ethiopia waliokamilisha muda wao wa kuhudumu humu nchini.
Akimuaga Balozi wa Ufaransa Arnaud Suquet, Ruto alielezea uhusiano wa karibu wa kidiplomasia kati ya Kenya na Ufaransa.
Alitaja mafanikio makubwa ya maandalizi ya Kongamano la Africa Forward Summit, lililohudhuriwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron mwezi Mei ambapo Balozi huyo aliwajibika pakubwa.
Aidha, ilikuwa mara ya kwanza kwa kongamano hilo kuandaliwa nje ya Ufaransa na barani Afrika, ambapo Kenya ilitia saini ushirikiano wa kibiashara ikiwa ni pamoja na ukarabati wa reli ya Nairobi kwa kima cha shilingi bilioni 12.5.
Balozi huyo anaondoka nchini baada ya kukamilisha muhula wake wa kuhudumu wa miaka minne.
Wakati uo huo, Ruto amemuaga Balozi wa Ethiopia humu nchini Bacha Debele Buta ambaye pia amekamilisha kipindi chake cha kuhudumu.