Mundubile akamatwa kwa madai ya uhaini

Mamlaka zilishutumu upinzani kwa kupanga uasi wa kutumia silaha, tuhuma ambazo upinzani ulikana.

Marion Bosire
1 Min Read

Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Brian Mundubile, ambaye alikuwa amejificha baada ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni wa urais, amezuiliwa kwa tuhuma za uhaini.

Matokeo rasmi ya uchaguzi wa tarehe 13 Agosti yalionyesha kuwa Rais aliye madarakani, Hakainde Hichilema, alishinda kwa kupata asilimia 60 ya kura, ikilinganishwa na asilimia 38 za Mundubile.

Siku moja baada ya uchaguzi, vikosi vya usalama vilivamia jumba moja katika mji mkuu Lusaka, lililohusishwa na Mundubile. Katika uvamizi huo, waziri wa zamani aliuawa na wanasiasa wengine kadhaa wakakamatwa.

Mamlaka zilishutumu upinzani kwa kupanga uasi wa kutumia silaha, tuhuma ambazo upinzani ulizikana.

Baada ya uvamizi huo, chama cha Mundubile, NRPUP, kilisema kwamba alienda eneo salama chini ya ulinzi wa taasisi ya kimataifa ya haki za binadamu kutokana na vitisho alivyokuwa akipokea.

Mgombea mwenza wa Mundubile, Makebi Zulu, pia alichukuliwa na polisi na kuwekwa kizuizini Alhamisi.

Wawili hao walikuwa wamehifadhiwa katika kituo cha Umoja wa Mataifa jijini Lusaka baada ya vikosi vya usalama kumuua waziri wa zamani na kuwakamata wanasiasa kadhaa.

Walizuiliwa baada ya rais kushinikiza Umoja wa Mataifa kuwakabidhi kwake.

Hichilema anatarajiwa kuapishwa kwa muhula wake wa pili tarehe 1 Septemba.

Share This Article