Wachochezi wa semi za chuki kujutia matendo yao, yaonya NCIC

Tume hiyo imeapa kuwawajibisha wanasiasa wenye hulka ya kutoa semi za chuki, ikiapa kufanya hivyo bila upendeleo.

Martin Mwanje
2 Min Read
Dkt. Kepha Omae - Mwenyekiti wa NCIC

Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, NCIC imeapa kukabiliana vikali na wanaoeneza semi za chuki nchini kote. 

Mwenyekiti wa tume hiyo. Dkt. Kepha Wamae ameahidi kuwa watawatema wanaoeneza semi za chuki bila upendeleo, bila kujali ikiwa wamo ndani au nje ya serikali.

“Lazima tushughulikie vichochezi vya migogoro kabla havijaongezeka, kukabiliana na semi za chuki na taarifa za upotoshaji,” alisema Dkt. Wamae wakati akisema tume hiyo tayari imeanza kuchukua hatua dhidi ya wahusika.

“Tumeanza kung’ata, na hili litafanywa kwa usawa lakini bila upendeleo inapokuja kwa suala la wanaoeneza semi za chuki.”

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa uchaguzi wa amani kuelekea 2027,  Dkt. Omae alisema NCIC imeazimia kuhamasisha mazungumzo na mardhiano ili kuziwezesha jamii kutatua migogoro kwa njia ya amani.

Matamshi yake yanawadia wakati ambapo tume hiyo imetuhumu watu kadhaa hasa wanasiasa kwa kuchochea semi za chuki.

Jana Jumatatu, mbunge wa Mukurweini John Kaguchia alifika mbele ya NCIC ili kuwajibishwa kuhusiana na semi alizozitoa zinazodhaniwa kuwa za chuki.

Wengine ambao wamejipata wakikwaruzana na tume hiyo kwa madai ya kutoa semi za chuki ni Mawaziri Aden Duale wa Afya na Geoffrey Ruku wa Utumishi wa Umma, na mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma.

Mashaka yameibuliwa kuhusiana na visa vinavyoongezeka vya utoaji wa semi za chuki kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

 

Share This Article