Wawili wakamatwa kuhusiana na mauaji ya Dkt. Mutiso

DCI inasema washukiwa hao wanahojiwa na kwamba hawajatambuliwa ili kutohujumu uchunguzi unaoendelea.

Martin Mwanje
1 Min Read
Dkt. Victoria Nthunya Mutiso aliyepigwa risasi na kuuawa Julai 29, 2026

Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI inasema watu wawili wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya Dkt. Victoria Nthunya Mutiso yaliyotokea jana Jumatano asubuhi. 

Dkt. Mutiso alifyatuliwa risasi na watu wasiojulikana katika eneo la Upper Hill jijini Nairobi.

Kwenye taarifa, DCI inasema maafisa wanaopeleleza mauaji hayo, wakisaidiwa na timu maalum za upelelezi na za kisayansi wamepata vidokezo muhimu kuhusu mauaji hayo kupitia mahojiano na mashuhuda, uchambuzi wa kisayansi na operesheni zilizolenga shabaha maalum.

“Kama sehemu ya jitihada hizi, wapelelezi wamepekua makazi ya watu wanaoshukiwa kuhusika katika mauaji hayo,” ilidokeza DCI..

“Operesheni hizo zilisababisha kupatikana kwa ushahidi unaochukuliwa kuwa muhimu kwa uchunguzi huo, na ambao kwa sasa unafanyiwa uchunguzi wa kina wa kisayansi.”

Awali, DCI iliashiria kuwa upelelezi wa awali unaashiria Dkt. Mutiso alikuwa ameitisha teksi alipofyatuliwa risasi katika mazingira ambayo ni ya kutatanisha.

 

Share This Article