Washukiwa wa wizi wa kimabavu, ubakaji wakamatwa

Wanaaminika kutekeleza visa mbali mbali vya uhalifu katika maeneo ya Yala, Siaya na Maseno.

Marion Bosire
2 Min Read

Washukiwa wa wizi wa kimabavu na ubakaji wamekamatwa na maafisa wa upelelezi wa jinai wa eneo la Kisumu Magharibi kwa ushirikiano na wenzao wa maeneo mbali mbali ya Nyanza.

Washukiwa hao wawili Fredrick Oduor Ongori na John Okumu Owidhi au Matools, wanaaminika kutekeleza visa mbali mbali vya uhalifu katika maeneo ya Yala, Siaya na Maseno.

Wanadaiwa kuvamia mwanamke mmoja na binamu yake waliokuwa wanaondoka eneo la burudani Mei 12, 2025, katika soko la Kisiani. Walikabili wawili hao waliokuwa wameabiri Tuktuk nje ya lango la kuingia nyumbani kwao katika kijiji cha Ongallo.

Wakiwa wamejihami kwa mapanga washukiwa walimkamata mwanamke huyo na kumwingiza kwenye gari walilokuwa wakitumia aina ya Toyota Axio la rangi ya kijivu lakini binamu yake akafanikiwa kukwepa.

Walimdhulumu kwa muda huku wakitaka awape pesa kupitia simu yake. Baadaye mwanamke huyo alipatikana katika eneo la Daraja Mbili kwenye barabara ya Kiboswa akiwa amebakwa na kupokonywa simu na bidhaa nyingine.

Wapelelezi walianzisha uchunguzi wakitumia taarifa za kijasusi walizokuwa wamepokea katika jiji la Kisumu ambapo walipata gari lililokuwa likitumiwa na washukiwa lenye nambari ya usajili KDA 019U.

Fredrick Oduor Ongori ndiye alikuwa dereva na anaaminika kuwa kiongozi wa genge la wahalifu. Alielekeza maafisa hadi mtaa wa mabanda wa Obunga ambapo mwenzake kwa jina John Okumu Owidhi au Matools naye alikamatwa.

Uchunguzi ulibaini kwamba wawili hao walitoroka jela na wako kizuizini huku uchunguzi ukiendelea ili kukamatwa wahalifu wenzao.

Website |  + posts
Share This Article