Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amesema serikali inatekeleza miradi ya maendeleo katika sehemu zote za nchi kwa usawa.
“Mageuzi ya Kenya yanajikita katika usambazaji wa miradi ya maendelo kwa usawa na kujumuishwa kwa vigezo vya kiuchumi na kijamii kwa ruwaza ya taifa,” alisema Prof. Kindiki.
Akizungumza kwenye ziara katika kaunti ya Samburu, Kindiki alisema chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA), kinasalia chenye nguvu na ambacho kimedumisha mtazamo wake wa kitaifa, akidokeza kiko wazi kwa Wakenya wote na wanaowania nyadhifa za kisiasa mwaka 2027.
Aliongeza kuwa chama hicho kinachoongozwa na Rais William Ruto, hakina ubaguzi na kimepeleka miradi ya maendeleo katika sehemu ambazo awali zilitengwa.
Kwenye ziara hiyo, Kindiki aliwapokea wanachama wapya waliojiunga na UDA kutoka vyama vingine vya kisiasa, akiwemo Mwenyekiti wa wanawake wa chama cha Jubilee Maison Leshoomo, mbunge wa zamani wa Samburu kaskazini Alois Lentoimaga na wawakilishi wadi sita wakiongozwa na kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti ya Samburu aliyechaguliwa na vyama vya Jubilee na KANU kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita.
“Tunapowapokea wanachama wapya kwa chama cha UDA, tunajivunia kwa hatua tulizopiga katika kutekeleza manifesto ya chama,” alisema Kindiki.
Gavana wa zamani wa Samburu Moses Lenolkulal pia alijiunga rasmi na chama cha UDA.
Naibu huyo wa Rais aliwahakikishia waliojiunga na chama hicho kuwa watahudumiwa kwa usawa, akisema wapiga kura ndio watakaochagua wale watakaowania na chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu ujao kupitia uteuzi huru na wa haki.
“Karibuni sana kwa chama cha UDA wenzangu,” alisema Kindiki.