Ruto asifu COMESA, asema imesaidia kuleta utangamano wa kikanda

Kenya imekuwa mwenyeji wa Kongamano la 24 la COMESA linaloendelea katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC. Rais William Ruto atapokezwa uenyekiti wa COMESA leo Alhamisi.

Martin Mwanje
1 Min Read
Rais William Ruto amelilimbikizia sifa Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na Kusini (COMESA) akisema limesaidia mno katika kukuza utangamano wa kikanda. 
Amelitaja kama umoja wa kikanda unaoleta mabadiliko ambao umehamasisha utangamano kwa kipindi cha miongo mitatu iliyopita.
“Mwaka huu inatimia miaka 30 ya kupigwa kwa hatua kubwa ya safari yenye mabadiliko ya COMESA kuelekea utangamano wa kikanda,” alisema Rais Ruto alipowaandalia dhifa Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka COMESA katika Ikulu ya Nairobi jana Jumatano.
Alisema nchi wanachama wa COMESA zinajivunia ujasiri, uthabiti, na ushirikiano ambao umepanua masoko, kubuni fursa na kuimarisha umoja katika kuzipiga dafrau changamoto.
Kulingana naye, matamanio ya pamoja ya COMESA yanaendelea kuchochea eneo hilo kuelekea umoja jumuishi na wenye ustawi.
Dhifa hiyo ilihudhuriwa na Marais Azali Assoumani wa Comoros na Emmerson Dambudzo Mnangagwa wa Zimbabwe, na Mawaziri Wakuu Russell Mmiso Dlamini wa Eswatini na Mustafa Madbouly wa Misri.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Mahmoud Youssouf na Katibu Mkuu wa COMESA Chileshe Mpundu Kapwepwe pia walikuwapo.
Kenya imekuwa mwenyeji wa Kongamano la 24 la COMESA ambalo linaendelea katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC.
Kenya itakabidhiwa uenyekiti wa COMESA leo Alhamisi, ikipokezwa kijiti hicho kutoka kwa Burundi.
Website |  + posts
Share This Article