Kipyegon afungua msimu kwa kupiga muda wa kasi

Kipyegon ametwaa ushindi kwa muda wa kasi duniani wa dakika 14 sekunde 24.14.

Dismas Otuke
2 Min Read

Bingwa wa zamani wa dunia katika mita 5,000 Faith Kipyegon, amefungua msimu wake kwa kuweka muda wa kasi katika mkondo wa kwanza wa mashindano ya Diamond League, ulioandaliwa Jumamosi mjini Shanghai,uchina.

Kipyegon ametwaa ushindi kwa muda wa kasi duniani wa dakika 14 sekunde 24.14.

Waethiopia Likina Amebaw na Senayet Getachew walinyakua nafasi za pili na tatu mtawalia.

Akizungumza baada ya ushindi wake Kipyegon amesema;”nahisi vizuri imekuwa mbio nzuri na mwanzo mwema wa msimu .Lengo langu limekuwa kupima uwezo wangu na kujua mahala pa kurekebisha ili kuendeleza ari hiyo.Sisemi sitaendela na mbio zangu za mita 1,500, bali nitashiriki zote pamoja na mita 5,000.”

Bingwa wa Olimpiki katika mita 3,000 kuruka viunzi na maji Faith Cherotich amemaliza wa pili katika fani hiyo kwa muda bora wa binafsi wa dakika 8 sekunde 51.48,nyuma ya bingwa wa zamani wa Olimpiki Mganda Peruth Chemutai aliyeweka rekodi mpya ya dakika 8 sekunde 51.47.

Bouzayani Marwa wa Tunisia ameambulia nafasi ya tatu.

Mshindi wa nishani ya shaba ya dunia ya mita 1500 Reynold Cheruiyot amemaliza wa pili katika mita 3,000, kwa kutumia dakika 7 sekunde 26.11, nyuma ya Mohamed Abdilaah wa Ujerumani aliyeibuka mshindi.

Adreas Almgren wa Uswidi amemaliza wa tatu mbele ya Wakenya Timothy Cheruiyot,Cornelius Kemboi, na Mathew Kipsang, waliochukua nafasi za 4,5 na 6 mtawalia.

Ferdinand Omanyala amechukua nafasi ya pili katika mita 100 kwa sekunde 9.98, nyuma ya Gift Leotlela, wa Afrika Kusini aliyemaliza kwa sekudne 9.97.

Share This Article