Omollo: Serikali itaangamiza makundi yote ya wahalifu

Aliwahimiza wananchi kushirikiana kwa karibu na maafisa wa usalama kwa kutoa habari na kuunga mkono juhudi za kudumisha usalama kwenye jamii.

Tom Mathinji
1 Min Read
Raymond Omollo - Katibu wa Usalama wa Taifa.

Serikali imesema itaangamiza makundi yote ya wahalifu, ili kulinda amani na kuzuia ghasia za kisiasa, huku taifa hili linapojiandaa kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2027.

Akizungumza katika wakilishi wadi ya Kendu Bay mjini, eneo bunge la Karachuonyo, kaunti ya Homa Bay, Katibu wa Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo, alionya kuwa makundi ya wahalifu hayana nafasi katika jamii.

Omollo alithibitisha kuwa serikali imejitolea kumaliza kikamilifu siasa za ghasia, akisisitiza kuwa uhalifu na ghasia hazitakubaliwa kuongoza siasa au uongozi wa taifa hili.

“Serikali itamaliza siasa za ghasia. Makundi ya wahalifu hayana nafasi katika jamii na tutaendelea kuchukua hatua za kuyaangamiza ili kuwalinda wananchi wanaozingatia sheria,” alisema Dkt. Omollo.

Aliwahimiza wananchi kushirikiana kwa karibu na maafisa wa usalama kwa kutoa habari na kuunga mkono juhudi za kudumisha usalama kwenye jamii.

Share This Article