Washukiwa wawili wamekamatwa kwa kuhusishwa na wizi wa kimabavu na ubakaji kufuatia ajali ya barabarani Kikuyu, kaunti ya Kiambu.
Kulingana na maafisa wa polisi, waathiriwa walihusika kwenye ajali ya barabarani karibu na shule ya upili ya wavulana ya Kikuyu, wakati wanaume wawili waliojisingizia kuwa wasamaria wema walijitokeza wakidai kuwasaidia.
Washukiwa hao Kevin Ndereba Kilonzo na Shaban Warui Zainab, walikamatwa katika eneo la Kamangu, Kikuyu.
Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ilisema wawili hao waliwashambulia wanandoa hao, wakawaibia huku wakiwalazimisha kutambua namba za siri za mfumo M-Pesa na kutuma pesa zote kabla ya kumbaka mwanamke huyo.
Baada ya tukio hilo kuripotiwa kwa maafisa wa polisi, kikosi cha maafisa kutka Makao Makuu ya DCI na wale wa eneo la Kikuyu walianza uchunguzi maramoja.
“Kupitia uchunguzi wa kisayansi, maafisa hao waliwafumania washukiwa hao Kevin Ndereba Kilonzo na Shaban Warui Zainab katika eneo la Kamangu, Kikuyu”, Ilisema Idara ya DCI kwenye ukurasa wa X.
Maafisa hao pia walipata simu zilizotumika kutuma pesa, na panga mbili zinazoaminika kutumika kwenye uovu huo.
Aidha, maafisa hao wamepanua uchunguzi wao wakimtafuta mshukiwa aliyechukua simu hizo zilizoibwa wakilenga kutambua uwezekano wa washukiwa hao kuhusika na visa vya ujambazi na uhalifu wa kimapenzi uliotekelezwa katika kaunti ndogo ya Kikuyu na viunga vyake.
Washukiwa hao wawili wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kikuyu wakisubiri kutambuliwa na waathiriwa kabla ya kufikishwa mahakamani.