Waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo Mutahi Kagwe, amezindua mpango unaolenga kuongeza maradufu uzalishaji wa zao la Bixa hadi tani 3,000 kila mwaka.
Akizungumza alipozuru kampuni ya utayarishaji Bixa kaunti ya Kwale, waziri huyo alisema hatua hiyo itabuni nafasi zaidi za ajira na kuongoza mapato katika maeneo ya mashinani.
Kagwe alisema serikali za kaunti za Pwani zitashirikiana kupanua kwa pamoja uzalishaji wa Bixa, kupitia usambazaji wa mbegu zilizoidhinishwa, huduma dhabiti za nyanjani, ufadhili nafuu wa fedha na kufanya zao hilo kuwa la mapato ya hali ya juu nchini Kenya.
“Kinachohitajika sasa ni kuongeza uzalishaji shambani. Kwa sasa kampuni ya uzalishaji wa Bixa nchini Kenya, huzalisha kati ya tani 1,000 na 1,400 kila mwaka, licha ya kuwa na uwezo wa kuzalisha tani 3,000 kila mwaka,” alisema Kagwe.
Waziri huyo alidokeza kuwa serikali itaongeza idadi ya wakulima wanaokuza Bixa kwa kutoa mbegu zaidi kupitia Halmashauri ya Kilimo na Chakula (AFA).
Kulingana na Kagwe, upanuzi wa kilimo cha Bixa hautabuni tu nafasi za ajira, lakini pia utaifaidi sekta za uchukuzi, utayarishaji na uuzaji wao hilo nje ya nchi.
Kwa sasa kampuni hiyo inatofa nafasi za ajira 150 za moja kwa moja, huku mamia ya wengine wakifaidika kupitia ukulima wa kandarasi, uchukuzi na usambazaji.
Mmea wa Bixa hutumika katika utengenezaji wa rangi asili ya chakula, bidhaa za urembo na dawa za kiasili.