Chansela wa kwanza wa kike wa UoN afariki

Aliyekuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Profesa Stephen Kiama alimtaja Dkt. Rattansi kuwa bingwa wa elimu mkarimu aliyebadilisha maisha ya maelfu ya wanafunzi.

Marion Bosire
2 Min Read

Chansela wa kwanza wa kike wa Chuo Kikuu cha Nairobi, UoN, Dkt. Vijoo Rattansi, amefariki.

Dkt. Rattansi alihudumu kama Chansela wa UoN mwaka 2013 hadi 2023 na alitambulika kwa mchango wake mkubwa katika kuendeleza elimu ya juu, shughuli za hisani na kuwalea viongozi wa baadaye.

Kifo chake kilitangazwa leo Alhamisi na kuzua wimbi la salamu za rambirambi kutoka kwa viongozi wa sekta ya elimu na wanafunzi wa zamani.

Aliyekuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Profesa Stephen Kiama alimtaja Dkt. Rattansi kuwa bingwa wa elimu ambaye ukarimu wake ulibadilisha maisha ya maelfu ya wanafunzi kupitia ufadhili wa masomo na ushauri wa kitaaluma.

“Nimepokea taarifa za kifo chake kwa huzuni kubwa,” alisema Prof. Kiama, akiongeza kuwa Dkt. Rattansi alisimama naye kwa dhati alipokuwa akipitia kipindi kigumu zaidi katika maisha yake ya uongozi.

Mbali na UoN, Dkt. Rattansi alikuwa Mwenyekiti wa Rattansi Educational Trust na Daisy Eye Cancer Fund, huku pia akihudumu katika bodi mbalimbali za mashirika ya hisani.

Alitambulika pia kwa umahiri wake katika uongozi wa taasisi, utatuzi wa migogoro, ukusanyaji wa fedha na maendeleo ya taasisi.

Katika hotuba zake za mahafali, aliwahimiza wahitimu kuwa na subira, unyenyekevu na ustahimilivu, akiwakumbusha kuwa kama punje za mahindi ya kupasuka, kila mtu hufanikiwa kwa wakati wake.

Rattansi aliwahi kutunukiwa tuzo ya Rais ya Order of the Grand Warrior, OGW mwaka 2006 na ameacha urithi mkubwa wa huduma, huruma na kujitolea kuendeleza elimu nchini Kenya.

Share This Article