Aisha Jumwa ahama UDA, kutangaza chama kipya hivi karibuni

Jumwa anasema atatangaza hivi karibuni chama kipya atakachojiunga nacho huku ripoti zikiashiria analenga kugombea Ugavana wa kaunti ya Kilifi.

Martin Mwanje
1 Min Read
Aisha Jumwa - Waziri wa zamani wa Masuala ya Jinsia

Waziri wa zamani wa Masuala ya Jinsia Aisha Jumwa ametangaza rasmi kukihama chama tawala cha UDA. 

Jumwa amekuwa akionyesha dalili za kukigura chama hicho, ila alikosa ujasiri wa kutangaza hilo moja kwa moja.

Mara nyingi, akionekana kukirushia chama hicho vijembe usijue hatima yake ya kisiasa ni ipi.

Lakini sasa, Jumwa ambaye pia aliwahi kuhudumu kama mwenyekiti wa Bodi ya Barabara nchini Kenya (KRB) kabla ya muhula wake kupigwa breki na mahakama, anasema ndoa yake na UDA sasa imefikia kikomo.

“Baada ya muda mwingi wa kutafakari, maombi ya dhati, na mashauriano yasiyohesabika na watu ninaohudumia, nimefanya moja ya uamuzi mgumu zaidi katika safari yangu ya kisiasa,” alisema Jumwa kwenye taarifa.

“Kuanzia leo, AISHAH JUMWA KATANA si tena mwanachama wa United Democratic Alliance (UDA).

Jumwa akiahidi kutangaza hivi karibuni chama atakachojiunga nacho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Ripoti zinaashiria Jumwa anapanga kugombea Ugavana wa Kilifi katika uchaguzi huo.

 

 

 

Share This Article