Gavana wa Samburu Lati Lelelit leo Ijumaa aliwaongoza viongozi wa kaunti hiyo kukutana na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi kupanga namna watakavyoshirikiana kuongeza kasi ya maendeleo katika kaunti hiyo.
Waliohudhuria mkutano huo ni viongozi wa mashinani kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa ikiwa ni pamoja na UDA, Jubilee na PNU, wakiwemo wawakilishi wadi (MCAs) na wabunge wa zamani na wanaohudumu kwa sasa.
Mathalan, Mwakilishi wa Wanawake wa zamani wa Samburu Maison Leshomo na mbunge wa zamani Alois Lentoimaga ni miongoni mwa waliohudhuria.

Wakati wa mkutano huo, viongozi hao walikubali kufanya kazi pamoja na utawala wa Kenya Kwanza kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
“Pia tulijadili hatua ambazo tunachukua katika kubadilisha Samburu na nchi nzima,” alisema Rais Ruto baada ya mkutano huo.
“Nilieleza kwamba Mfuko wa Kitaifa wa Miundombinu ulioanzishwa hivi karibuni utatekeleza jukumu muhimu katika uendelezaji wa miundombinu, uhifadhi wa maji na uzalishaji wa nishati.”

Viongozi kutoka maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakikutana na Rais Ruto katika Ikulu ya Nairobi ambapo ametumia fursa hiyo kuwaelezea mipango mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kuu kwa manufaa ya raia.
Waangalizi wa mambo wanaiona hatua hiyo kuwa mbinu ya Rais kutafuta uungwaji mkono kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.