Wanaume watatu nchini Nigeria wamehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kukiri makosa yanayohusiana na utekaji wa makumi ya wanafunzi na walimu katika jimbo la Oyo, kusini-magharibi mwa nchi.
Watuhumiwa hao walikiri kuficha taarifa kuhusu watu waliohusika na mashambulizi hayo, na pia kukubali kuwa wanachama wa kundi linalohusishwa na Boko Haram.
Hukumu hiyo imekuja karibu wiki mbili baada ya mamlaka kutangaza kuwa wanafunzi na walimu 44 waliotekwa nyara katika mashambulizi ya kuratibiwa dhidi ya shule tatu wilayani Oriire mwezi Mei waliokolewa.
Matukio hayo ya utekaji yalisababisha maandamano kutoka kwa wazazi, vyama vya walimu na mashirika ya kutetea haki za binadamu, ambayo yalitaka serikali kuimarisha usalama wa shule.
Katika miaka ya hivi karibuni, utekaji wa watu kwa ajili ya kudai fidia umekuwa ukiongezeka nchini Nigeria, huku makundi yenye silaha yakilenga maeneo yenye ulinzi hafifu kama vile shule, makanisa, misikiti na vijiji vya mbali.
Nigeria inaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali za kiusalama, zikiwemo magenge ya wahalifu yanayojulikana kama “bandits”, ambayo hujihusisha na uporaji na utekaji wa watu kwa ajili ya kudai fidia.
Nchi hiyo pia inakabiliwa na uasi wa makundi ya wanamgambo wa Kiislamu, migogoro ya ardhi kati ya jamii mbalimbali, pamoja na machafuko yanayochochewa na makundi yanayotaka kujitenga katika baadhi ya maeneo ya nchi.
Taarifa ya BBC