Nyota wa muziki wa Uganda Jose Chameleone anatarajiwa kuheshimiwa katika awamu ya nne ya Bongo Flava Honors, na kuwa msanii wa kwanza kutoka nje ya Tanzania kutambuliwa na jukwaa hilo.
Jukwaa hilo, lilianzishwa kwa lengo la kuwatambua na kuwapongeza waanzilishi na magwiji waliounda na kukuza muziki wa Bongo Flava.
Akizungumza baada ya kumpokea Chameleone na mamake mzazi jana, Joseph Mbilinyi mmoja wa wadau wakuu wa Bongo Fleva Honors alisema kwamba Chameleone ameshirikiana na wasanii kadhaa wa Tanzania hivyo anastahili tuzo hiyo.
Chameleone, mwanzilishi wa lebo ya Leone Island atatunukiwa kwa mchango wake katika muziki wa Afrika Mashariki na nafasi yake katika kueneza muziki wa mijini wenye ladha ya Kiswahili nje ya mipaka ya Tanzania.
Ushawishi wa Chameleone katika ukanda huu ni wa zaidi ya miongo miwili, huku nyimbo zake zikimjengea umaarufu mkubwa miongoni mwa mashabiki wa Bongo Flava.
Bongo Flava Honors awamu ya 4 itaandaliwa Julai 31, 2026 ndani ya Super Dome, Masaki, Dar es Salaam Tanzania na Mbilinyi ameahidi tamasha ya kipekee.
Kutunukiwa kwa Chameleone kunaashiria kuongezeka kwa ushawishi wa Bongo Flava katika ukanda wa Afrika Mashariki na umuhimu wake nje ya Tanzania, huku ikiwakutanisha wanamuziki wa vizazi tofauti waliochangia ukuaji wa muziki wa eneo hili.
Wasanii waliowahi kutunukiwa katika Bongo Flava Honors ni pamoja na Master Sugu, Jay Moe, Lady Jaydee, TMK Wanaume Halisi na Profesa Jay.