Kenya na Uingereza zarejelea mafunzo ya pamoja ya jeshi

Waziri wa mambo ya nje Musalia Mudavadi amesema hatua hiyo inaonyesha ushirikiano imara na wa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili.

Marion Bosire
1 Min Read
Musalia Mudavadi - Mkuu wa Mawaziri

Serikali imekaribisha hatua ya kurejelewa kwa mafunzo ya pamoja ya kijeshi kati ya Kenya na Uingereza katika Kituo cha Mafunzo cha Jeshi la Uingereza nchini Kenya, BATUK.

Katika taarifa, mkuu wa mawaziri na waziri wa mambo ya nje Musalia Mudavadi amesema hatua hiyo inaonyesha ushirikiano imara na wa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili, unaojengwa kwa kuheshimiana na kujitolea kwa pamoja katika kudumisha amani na usalama.

Mudavadi amesema ushirikiano wa ulinzi kati ya Kenya na Uingereza unaendelea kuunga mkono maslahi ya kitaifa ya Kenya kwa kuimarisha uwezo wa Jeshi la Kenya, KDF, kukuza utulivu wa kikanda, na kuleta fursa za kiuchumi kwa jamii zinazoishi karibu na kituo hicho cha mafunzo.

Amesema uamuzi huo unaonyesha kuwa washirika wanaoaminiana wanaweza kushughulikia changamoto kupitia mashauriano yenye kujenga na nia njema.

Mkuu huyo wa mawaziri amesisitiza dhamira ya Kenya ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa ulinzi na Uingereza, akisema ushirikiano huo unalenga kuleta manufaa ya kudumu kwa mataifa hayo mawili na wananchi wake.

Kituo cha Mafunzo cha Jeshi la Uingereza nchini Kenya, kilichopo Kaunti ya Laikipia, kimekuwa kikihudumia mafunzo ya pamoja ya kijeshi kwa miongo kadhaa, yakilenga kuimarisha uwezo wa ulinzi na utayari wa kukabiliana na changamoto za kiusalama.

Share This Article