Emmanuel Kiprono, alishinda dhahabu ya mbio za mita 3000 katika siku ya tatu ya mashindano ya Riadha Duniani kwa chipukizi chini ya umri wa miaka 20 mjini Oregon,Marekani.
Kiprono alitimka mbio hizo kwa dakika 7 sekunde 28.28,ikiwa rekodi mpya ya mashindano hayo,akikosea sekunde 9 pekee afikie rekodi ya Dunia ya mwaka 2016, iliyowekwa na Mwethiopia Yomif Kejelcha.
Mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu katika shule ya St Francis Kimuron,aliongoza kutoka mwanzo hadi mwisho na kuinyakua Kenya Dhahabu ya pili kwenye mashindano hayo.
Alois Abraham wa Ufaransa alishinda fedha kwa dakika 7 sekunde 47.79, huku Ojira Honda wa Japan, akiridhia shaba kwa muda wa dakika 7 sekunde 48.49.
Awali Anatasha Cheptoo alikuwa ameshinda nishani ya shaba katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji.
Ethiopia ilinyakua medali za dhahahbu na fedha kupitia kwa Almaz Yahannis na Wosane Asefa mtawalia.
Kenya ni ya pili kwenye msimamo wa nsihani kwa dhahabu 2 fedha 1 na shaba 2.
Wenyeji Marekani wanaongoza kwa dhahabu 5 na fedha 5.