Maxine Wahome aondolewa hatia katika kesi ya Asad Khan

Marion Bosire
2 Min Read

Dereva wa mashindano ya uendeshaji magari, Maxine Wahome, ameondolewa hatia katika kesi ya mauaji ya mpenzi wake na dereva mwenza wa mashindano ya magari Asad Khan.

Hii ni baada ya mahakama kuu kubaini kuwa upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi wa kutosha.

Katika uamuzi uliotolewa leo Jumanne, Jaji Lilian Mutende alisema ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka haukumhusisha Wahome moja kwa moja na majeraha yaliyosababisha kifo cha Khan.

Jaji aliamua kuwa ushahidi wa mazingira uliotegemewa na serikali haukumbainisha Wahome pekee kama aliyesababisha majeraha hayo.

Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 29 ukidai kuwa Wahome na Khan ndio waliokuwa pekee ndani ya nyumba wakati wa tukio hilo.

Hata hivyo, mahakama ilielezwa kuwa hakuna aliyeshuhudia jinsi Khan alipata majeraha, huku wachunguzi wakipata damu kwenye vipande vya kioo kilichovunjika lakini bila ushahidi wa kisayansi unaohusisha vitu vingine vilivyopatikana eneo la tukio na majeraha hayo.

Ushahidi wa kitabibu pia ulionyesha kuwa baadhi ya majeraha ya Khan huenda yalisababishwa na kuanguka kwenye ngazi.

Afisa mpelelezi alikiri pia kuwa hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja unaothibitisha kuwa Wahome ndiye alisababisha majeraha yaliyosababisha kifo.

Jaji Mutende pia aliamua kuwa mwenendo wa Wahome baada ya tukio, kama kutomtembelea Khan hospitalini au kuhudhuria mazishi yake, hauwezi kuthibitisha kuwa alikuwa na hatia ya jinai.

Asad Khan alifariki Disemba 18, 2022 akipokea matibabu jijini Nairobi.

Share This Article