Wanasheria kususia mahakama kulalamikia ufisadi

Mpango huo wa siku moja unalenga kupinga ufisadi na utovu wa maadili ndani ya Idara ya Mahakama.

Marion Bosire
1 Min Read

Chama cha Wanasheria Nchini Kenya,LSK kimetangaza mpango wa kususia huduma za mahakama kote nchini siku ya Jumatano, tarehe 22 Julai 2026, kupinga ufisadi na utovu wa maadili ndani ya Idara ya Mahakama.

Chama hicho kinawashutumu baadhi ya maafisa wa mahakama kwa matumizi mabaya ya mamlaka, mienendo isiyo ya kimaadili, na vitendo ambavyo vimedhoofisha imani ya umma katika mfumo wa utoaji haki.

Kimetaja pia kucheleweshwa kwa usimamizi wa kesi, uzembe katika sajili za mahakama, na hitilafu za mara kwa mara katika mifumo ya uwasilishaji wa nyaraka kwa njia ya kielektroniki kuwa mambo yanayodhalilisha hadhi ya taaluma ya mawakili.

Akizungumza mjini Machakos baada ya kukutana na viongozi wa Kanda ya Kusini Mashariki pamoja na wanachama wa Tawi la Machakos, Rais wa LSK, Charles Kanjama, alisema mpango huo wa kususia mahakama kwa siku moja utawazuia wanachama kushiriki katika kusikilizwa kwa kesi na maombi mahakamani.

Kanjama alifafanua kuwa uwasilishaji wa kesi mpya utaendelea kama kawaida, huku kutajwa kwa kesi na maombi yanayohusu amri za muda kukiendelea tu kwa madhumuni ya kupata tarehe mpya za kusikilizwa au kuongeza muda wa amri hizo za muda.

Share This Article