Utata ambao umezingira uongozi wa Chuo Kikuu cha Nairobi kwa muda sasa unatazamiwa kufikia kikomo baada ya Mhandisi Prof. Ayub Gitau kutawazwa kuwa Makamu Chansela mpya wa chuo hicho.
Yeye ni Makamu Chansela wa tisa kuwahi kuhudumu katika wadhifa huo.
Hafla ya kumtawaza Prof. Gitau ilifanyika leo Ijumaa katika Ukumbi wa Taifa chuoni hapo.
Aliteuliwa kwenye wadhifa huo na Baraza la Chuo Kikuu cha Nairobi na anachukua wadhifa ambao Prof. Margaret Jesang Hutchinson amekuwa akikaimu.
Tangu kuondoka kwa marehemu Prof. George Magoha kwenye wadhifa huo, Chuo Kikuu cha Nairobi kimekumbwa na mizozo ya uongozi ambayo ilitishia kukisambaratisha chuo hicho kinara.