EACC na DPP kushirikiana kupambana na ufisadi, utakatishaji fedha

Martin Mwanje
1 Min Read

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) zimesisitiza dhamira yao ya kuboresha  ushirikiano ili kuimarisha uchunguzi na ufunguaji wa mashtaka katika kesi za ufisadi na utakatishaji fedha. 

Pande hizo mbili ziliafikiana hayo wakati wa mkutano ulioleta pamoja uongozi wa taasisi hizo.

Mwenyekiti wa EACC Dkt. David Oginde alitumia fursa hiyo kusema ufisadi unasalia changamoto kuu kwa ustawi wa nchi hii kwani unafifisha imani ya umma na kudunisha utoaji huduma kwa raia.

Ni kwa misingi hiyo ambapo mwenyekiti wa EACC Abdi Mohamud alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya sekta za haki ni kigezo muhimu cha kikatiba na kinachohitajika ili kufikia matokeo yenye tija.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga alisema mkutano huo ulitoa fursa kwa taasisi hizo mbili kuimarisha utoaji huduma kwa kuboresha ubora wa uchunguzi na ufunguaji mashtaka.

Taasisi hizo zimeahidi kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao ya kikatiba, zikitaja ushirikiano huo kuwa muhimu katika kuimarisha uwajibikaji na upatikanaji wa haki nchini.

Share This Article