Ruto: Kikosi maalum cha polisi kuimarisha usalama Nairobi

Rais amesema kikosi hicho kitasaidia kuimarisha usalama wa raia, kuongeza uaminifu kati ya jamii na maafisa wa kutekeleza sheria, na kujenga maeneo salama kwa wote.

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto ameelezea kuridhishwa kwake na hatua iliyopigwa katika kuanzisha kikosi maalum cha polisi eneo la Nairobi kwa lengo la kuimarisha usalama wa wakazi wa eneo hilo. 

Kikosi hicho kitaanzishwa hivi karibuni chini ya Mpangokazi wa Polisi wa Eneo la Nairobi na kuweka msingi wa mfumo wa polisi unaotoa kipaumbele zaidi kwa uratibu, uwajibikaji na jamii katika eneo lote la Nairobi.

“Pamoja, tutaimarisha usalama wa raia, kuongeza uaminifu kati ya jamii na maafisa wa kutekeleza sheria, na kujenga maeneo salama kwa wote,” alisema Rais Ruto wakati wa mkutano na maafisa wa ngazi ya juu katika sekta ya ulinzi.

Maafisa hao walijumuisha Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen na uongozi wa Huduma ya Taifa ya Polisi ukiongozwa na Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja pia alihudhuria mkutano huo.

Rais Ruto alielezea kuwa mpangokazi huo utatoa kipaumbele kwa jamii katika utoaji huduma za ulinzi kwa kuleta pamoja wakazi, viongozi wa jamii, Huduma ya Taifa ya Polisi, serikali ya kaunti ya Nairobi na washikadau wengine.

Hilo litafikiwa kwa kutambua kwa pamoja vipaumbele vya usalama, kuimarisha uangalizi na kuendeleza suluhu za eneo la Nairobi kupitia mashauriano na ushiriki wa umma.

Eneo la Nairobi limekabiliwa na changamoto za usalama siku zilizopita huku visa vya uporaji vikikithiri hasa katikati ya jiji.

Share This Article