Serikali imetoa wito kwa Wakenya kutumia vyema haki zao za kikatiba na kwa njia ya amani, ikionya kuwa ghasia, uharibifu wa mali na kutozingatia sheria, ni tisho kwa udhabiti wa taifa na maendeleo ya kiuchumi.
Akizungumza wakati wa sherehe ya kuwatuza wanafunzi wa shule ya Chinga Boys kaunti ya Nyeri, Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo, alisema uhuru wa kikatiba unapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia sheria pamoja na kuheshimu haki ya wengine.
Alidokeza kuwa uzingatiaji wa sheria ni muhimu kwa ulinzi wa demokrasia, mshikamano wa kitaifa na kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya taifa hili.
“Katiba inampa kila Mkenya haki ya kujieleza na kuandamana, lakini haki hizo zinapaswa kutekelezwa kwa njia ya amani, kwa kuzingatia sheria na kuheshimu haki za wengine,” alisema Dkt. Omollo.
Alikashifu ghasia, uporaji, uharibifu wa mali na mashambulizi dhidi ya watu wasio na hatia wakati wa maandamano, akidokeza kuwa tabia za uhalifu hazipaswi kuchukuliwa kama kutekeleza haki ya kikatiba.
“Kuna tofauti kubwa kati ya maandamano ya amani na shughuli za uhalifu. Uteketezaji wa biashara, uporaji wa mali, kuwashambulia watu na uharibifu wa miundombinu ya umma hazina manufaa yoyote,” aliongeza Katibu huyo.
Aidha, alitoa wito kwa viongozi wa kisiasa, wazazi, walimu, viongozi wa dini na jamii kuzingatia uwajibikaji, heshima na utangamano wa amani,