Rais Ruto kuwakilisha Afrika kwenye mkutano wa G7 Ufaransa

Rais Ruto anatarajiwa kuimarisha ushirikiano imara kati ya Afrika na chumi bora zaidi duniani katika maswala ya biashara, miundombinu, nishati na uvumbuzi.

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron kwenye kongamano la Africa Forward Jijini Nairobi.

Rais William Ruto, atasafiri Jumatatu usiku kuelekea Evian, Ufaransa kwa mwaliko wa Rais Emmanuel Macron, kushiriki kwenye mkutano wa viongozi wa G7, ambako atawakilisha bara Afrika.

Kwenye taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed Jumatatu jioni, mwaliko huo unaashiria ukuaji wa ushawishi wa Kenya katika maswala ya kimataifa na ujasiri wa uongozi wa Rais Ruto katika maswala yanayoathiri bara Afrika.

“Kwenye mkutano huo, kiongozi huyo wa taifa anatarajiwa kuwasilisha msimamo wa Afrika ulioafikiwa katika kongamano la  Africa Forward lililoandaliwa Jijini Nairobi mwezi Mei, ambalo lilibuni ajenda ya pamoja kuhusu mageuzi ya kiuchumi, kifedha, hatua ya kukabiliana na Tabianchi na maendeleo ya kidijitali,” ilisema taarifa hiyo.

Aidha, kongamano hilo litatoa fursa muhimu kwa Rais Ruto kupigia debe maswala ya Afrika ambayo ni marekebisho kwenye mfumo wa kifedha, upatikanaji wa uwekezaji na kutekelezwa kwa mapendekezo ya kongamano la Africa Forward kuhusu fedha  ili kutoa fursa kwa ukuaji, upatikanaji wa nafasi za kazi na fursa zilizopanuliwa za kifedha kwa wafanyabiashara wa Kenya.

Rais Ruto pia anatarajiwa kuimarisha ushirikiano imara kati ya Afrika na chumi bora zaidi duniani katika maswala ya biashara, miundombinu, nishati na uvumbuzi.

Wanaotarajiwa kuhudhuria kongamano hilo ni pamoja na Rais  Emmanuel Macron (Ufaransa), Rais Donald Trump (Marekani), Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney,  Chancellor Friedrich Merz wa Ujerumani, Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, Waziri Mkuu wa Japan Shigeru Ishiba, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, Rais wa Baraza la Ulaya António Costa na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen, miongoni mwa viongozi wengine waalikwa.

Share This Article