Wazee wa Mau Mau wakemea vurugu za kisiasa

Wanaonya kuwa hali hiyo inatishia amani ya taifa na nafasi ya demokrasia.

Marion Bosire
2 Min Read

Baadhi ya wanachama wa kundi lililopigania uhuru, Mau Mau wamekemea ongezeko la matukio ya vurugu za kisiasa na matumizi ya makundi ya wahuni wanaokodishwa kuvuruga mikutano ya umma.

Wazee hao wanaonya kuwa hali hiyo inatishia amani ya taifa na nafasi ya demokrasia.

Walieleza wasiwasi kuhusu hali hiyo wakisema vurugu hizo zimesababisha Wakenya wengi kupoteza maisha, kujeruhiwa, na familia nyingi kupata hasara baada ya mali zao kuharibiwa.

Wakizungumza na wanahabari katika kaunti ya Kiambu, wana Mau Mau hao walitaja matukio ya hivi karibuni huko Ol Kalou na Kisumu, ambako mikutano ya kisiasa ilivurugwa na makundi yenye silaha.

Walirejelea hasa jaribio la kuvuruga mkutano wa Linda Mwananchi Kisumu na kuhudhuriwa na Gavana wa Siaya, James Orengo na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, ambapo watu waliovaa barakoa walidaiwa kujaribu kuvuruga mkutano huo.

Wapigania uhuru hao walisema Kenya haipaswi kurejea katika kipindi ambacho ushindani wa kisiasa ulitawaliwa na vurugu na vitisho.

Walisisitiza kuwa kujitolea kwao wakati wa kupigania uhuru kulilenga kuijengea Kenya taifa lenye amani na demokrasia, sio taifa ambalo wananchi wanaendelea kupoteza maisha kutokana na tofauti za kisiasa.

Wazee hao waliwataka viongozi wa kisiasa kutoka pande zote kukumbatia mazungumzo na kuvumiliana, wakisema kuwa ushirikiano wa amani ndio njia pekee endelevu ya kutatua migogoro ya kisiasa.

Walionya kuwa kuendelea kwa vitendo vya vurugu na uvunjaji sheria kunaweza kutumbukiza taifa katika hali ya sintofahamu na kudhoofisha mafanikio yaliyopatikana katika demokrasia.

Pia walisihi mashirika ya usalama kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaohusika kupanga au kufadhili vurugu za kisiasa, bila kujali misimamo yao ya kisiasa.

Wakati huo huo, wana Mau Mau wamekubaliana na uamuzi wa Rais William Ruto wa kutia saini kuwa sheria Mswada wa Hazina ya Utajiri wa Taifa, wakieleza matumaini kwamba sheria hiyo itasaidia kulinda utajiri wa asili wa nchi na kuchochea ustawi wa uchumi wa muda mrefu kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Share This Article