Washukiwa 6 waliokamatwa kutokana na madai ya kushambulia msafara wa mrengo wa Linda Mwananchi huko Keumbu walikosa kusomewa mashtaka baada ya kufikishwa katika mahakama ya Kisii.
Hii ni baada ya upande wa mashtaka na afisa aliyewakamata kukosa kufika mahakamani.
Hakimu Mkuu Mkazi Caroline Cheruiyot aliagiza washukiwa hao kurejeshwa korokoroni hadi wakati ambapo faili yao itakapokuwa tayari.
Washukiwa walikamatwa wikendi iliyopita kufuatia uchunguzi uliofanywa na afisa anayesimamia kituo cha Keumbu na Idara ya Upelelezi wa Jinai huko Kisii ya Kati.
Msafara wa mrengo wa Linda Mwananchi ulirushiwa mawe na kundi la watu Ijumaa wiki iliyopita wakati viongozi wa mrengo huo walipotembelea eneo la Kisii.
Mtu mmoja alifariki wakati wa vurugu hizo huku wengine wakijeruhiwa vibaya.
Taarifa ya Mercy Amoh