Polisi, jeshi watanda kuzuia maandamano 7/7 Tanzania

radiotaifa
2 Min Read

Usalama unaendelea kuimarishwa kwenye miji mikubwa nchini Tanzania ambapo kumeshuhudiwa maafisa wa polisi na jeshi wenye silaha wakifanya doria, huku serikali ikionya kuwa itachukua hatua dhidi ya mtu yeyote atakayehamasisha vurugu siku hiyo.

Maafisa hao wameonekana kwa wingi katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenye mizunguko ya barabara na mitaa katika jiji kuu la kibiashara la Dar es Salaam na miji mingine, hali ambayo wengi wanadai kuwa si ya kawaida, baadhi yao wakisema ni njia ya kudhibiti maandamano yanayopangwa kufanyika siku ya Jumanne.

Hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii, wanaharakati wamekuwa wakihamasisha kufanyika maandamano siku ya Jumanne, kushinikiza kuwepo kwa uhuru wa kisiasa na uwajibikaji kufuatia matukio ya mauaji yaliyotokea kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Maandamano hayo yanayodaiwa kupangwa yanakuja wakati ambapo serikali imedai kuwa na taarifa za kiintelijensia kuwa kuna watu wanaopanga kudhuru baadhi ya viongozi, wananchi pamoja na kuharibu mali.

Wakati hayo yakiedelea, Jumanne ni siku ambayo ni ya kitaifa ya Maonesho ya Biashara ya Dar es Salaam, maarufu kama Saba Saba, ambayo ni miongoni mwa maonesho makubwa zaidi ya kibiashara nchini Tanzania.

Mitandao ya kijamii sababu ya maandamano?

Serikali imedai kuwa kuna raia ambao wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuhamasisha maandamano au vurugu hivyo imejipanga kuchukua hatua kudhibiti hali yoyote ile itakayojitokeza.

Kwa mujibu wa viongozi mbalimbali wa Serikali ya Tanzania, uhamasishaji mkubwa umekuwa ukifanyika kupitia mitandao ya kijamii na wanaharakati ambao wenye lengo la kuleta vurugu.

Japokuwa wanaharakati hao mitandaoni wamekuwa wakisema lengo lao ni kudai mageuzi ya kidemokrasia, haki kwa watu waliouawa wakati wa machafuko yaliyofuatia uchaguzi pamoja na uwajibikaji kwa viongozi wa Serikali na vyombo vya dola.

Taarifa ya BBC

Share This Article