Kuimarisha maandalizi dhidi ya Ebola ni muhimu, ahimiza Duale

Martin Mwanje
2 Min Read
Aden Duale - Waziri wa Afya

Kuna haja kwa Kenya kuimarisha zaidi maandalizi dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola uliotokea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Visa kadhaa vya ugonjwa huo pia vimeripotiwa katika nchi jirani ya Uganda.

Waziri wa Afya Aden Duale amesema maandalizi dhidi ya ugonjwa huo ni muhimu ili kuhakikisha nchi hii haitajipata pabaya ikiwa mlipuko wa ugonjwa huo utatokea nchini.

“Kenya inaongeza hali endelevu ya utayari dhidi ya mlipuko wa kikanda wa Ugonjwa wa Ebola unaosababishwa na Virusi aina ya Bundibugyo (BEVD), na kuthibitisha tena kuwa maandalizi yanasalia ngao imara dhidi ya matishio yanayoibuka ya afya ya umma licha ya kutokuwa na visa vyovyote vilivyothibitishwa,” amesema Duale.

Waziri aliyasema hayo leo Alhamisi wakati wa mkutano wa mashauriano wa ngazi ya juu uliowaleta pamoja wawakilishi kutoka serikali ya Marekani, washirika na washikadau wengine ili kupitia upya hali ya maandalizi ya Kenya dhidi ya ugonjwa wa Ebola.

Aidha, mkutano huo ulikusudia kuimarisha uratibu na kuainisha msaada kuelekea kuimarisha uwezo wa nchi hii kuzuia, kutambua na kukabiliana na mlipuko wowote unaoweza kutokea nchini.

Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Umma humu nchini (KNPHI), kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Visa, imetambua kaunti 25 zilizo katika hatari kubwa ya kukumbwa na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola.

Serikali ikisema kuna umuhimu wa maandalizi madhubuti kuongezwa katika kaunti hizo wakati pia msaada wa kiufundi na utengaji rasilimali zaidi vikitolewa katika kaunti hizo.

Watu zaidi ya 300 wameripotiwa kufariki nchini DRC kutokana na ugonjwa wa Ebola huku visa 1,000 vikiripotiwa.

Katika nchi jirani ya Uganda, vifo 2 vimeripotiwa huku angalau visa 20 vikiripotiwa.

Kenya haijaripoti kisa chochote cha ugonjwa wa Ebola.

 

Share This Article