Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ametoa wito wa kuimarishwa kwa uaminifu kati ya wananchi, taasisi na serikali hususan wakati huu ambapo kuna changamoto zilizoibuka kutokana na enzi ya kidijitali.
Ametaja hatua hiyo kuwa muhimu hasa wakati huu ambapo kumeibuka changamoto za taarifa za upotoshaji na kupunguka kwa imani ya umma.
“Uaminifu ndio msingi ambapo taasisi thabiti, nchi imara za kidemokrasia na zilizostawi kiuchumi hujengwa,” alisema Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.
“Kenya inahamasisha uendelezaji wa mpangokazi ambao utaimarisha uwezo wa taasisi muhimu zinazokuza uwazi, uwajibikaji na imani ya umma wakati ukilinda maadili ya kidemokrasia katika enzi ya kidijitali.”
Waziri Mudavadi aliyasema hayo wakati wa Mkutano wa Mashauriano wa Taasisi za Udhibiti nchini Kenya juu ya Kongamano la Uaminifu Duniani 2026 litakaloandaliwa nchini kati ya Oktoba 22-23 mwaka huu.
Kongamano hilo litaangazia uimarishaji wa uadilifu wa taarifa, taasisi za kidemokrasia, maongozi baina ya vizazi, uaminifu kama mali ya kiuchumi na mustakabali wa ushirikiano wa pande nyingi na wa kimataifa.