Kesi dhidi ya wanafunzi 8 wa Utumishi Girls kutajwa leo Jumatano

Martin Mwanje
1 Min Read
Wanafunzi wanaoshukiwa kusababisha mkasa wa moto Utumishi Girls Academy walipofikiwa mahakamani awali

Wanafunzi 8 wanaoshukiwa kusababisha mkasa wa moto katika shule ya Utumishi Girls Academy mjini Gilgil, kaunti ya Nakuru mwishoni mwa mwezi Mei watafikishwa kizimbani leo Jumatano.

Kesi dhidi yao itatajwa katika Mahakama Kuu ya Kibera watakapofikishwa mbele ya Jaji Diana Kavedza.

Wanafunzi hao wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji.

Awali, mahakama hiyo iliagiza wanafunzi hao kufanyiwa uchunguzi wa kiakili katika Hospitali ya Akili ya Mathare.

Agizo hilo lilitolewa na Naibu Msajili wa mahakama hiyo Barbara Akinyi wakati washukiwa walipofika mbele yake kwa njia ya mtandao.

Akinyi aliagiza matokeo ya uchunguzi huo kuwasilishwa kwa mahakama kabla ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Kadhalika, mahakama iliagiza washukiwa kufanyiwa uchunguzi na afisa wa watoto katika makazi ya watoto ya Kabete kabla ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Wanafunzi 16 walifariki wakati mkasa wa moto ulipotokea katika shule ya Utumishi Girls Academy Mei 28 huku wanafunzi wengine 79 wakijeruhiwa.

Uchunguzi ulibaini bweni la shule hiyo lilitetekezwa kimakusudi na kusababisha maafa hayo, mkasa unaoshukiwa kusababishwa na wanafunzi hao.

Serikali imeapa kuwachukulia hatua kali wanafunzi watakaopatikana wakijiusisha katika uovu kama huo siku zijazo.

Share This Article