Maafisa wa umma wanaotaka kugombea nyadhifa mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu ujao wanapaswa tu kuruhusiwa kujiuzulu baada ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu.
Seneta wa Narok Ledama Olekina anasema hatua hiyo itawaruhusu watakaoshinda viti mbalimbali kwenye uchaguzi huo kuhudumu katika nyadhifa zao mpya wakati wale walioshindwa wakirejelea kazi zao katika utumishi wa umma.
“Maafisa wa umma wanaotaka kugombea kwenye uchaguzi hawapaswi kutakiwa kujiuzulu mapema. Ingawa Katiba inahakikisha haki za kisiasa, pia inahitaji maafisa wa umma kutoegemea upande wowote, kudumisha uadilifu, na imani ya umma afisini,” amesema Olekina.
“Mbinu yenye usawa ni kuwaruhusu kuendelea kuhudumu hadi wachaguliwe na kisha kujiuzulu baada ya kuchaguliwa, badala ya kuwataka kujiuzulu mapema na hivyo yamkini kuwaadhibu wale ambao hawatachaguliwa.”
Kwenye ratiba yake kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC imewataka maafisa wote wa umma wanaopanga kugombea nyadhifa mbalimbali za uongozi mwakani kujiuzulu kufikia Februari 9.
Kwa mujibu wa IEBC, kampeni rasmi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 itaanza Mei 29 na kumalizika Agosti 7, 2027 siku tatu kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu.
Kampeni hizo zitafanyika kati ya saa moja asubuhi na saa kumi na mbili jioni.
Shughuli ya kuwasajili wapiga kura nayo itafungwa Juni 12 mwakani, kwa mujibu wa ratiba ya IEBC.
Uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 utaandaliwa Agosti 10 na tayari wanasiasa wameanza kufanya kampeni hata kabla ya kipenga rasmi cha kufanya hivyo kupulizwa.