Kenya imewachunguza wasafiri 140,000 dhidi ya ugonjwa wa Ebola

Waziri wa afya Aden Duale amewahakikishia Wakenya kuwa hakuna kisa chochote cha ugonjwa wa Ebola kimenakiliwa nchini Kenya.

Tom Mathinji
1 Min Read
Aden Duale - Waziri wa Afya.

Kenya imewapima wasafiri zaidi ya 140,000 ambao wametoka maeneo yaliyoathiriwa na ugonjwa wa Ebola, huku ikichunguza visa 100 ambavyo havikupatikana na ugonjwa huo.

Kwenye taarifa siku ya Alhamisi, Waziri wa afya Aden Duale amewahakikishia Wakenya kuwa hakuna kisa chochote cha ugonjwa wa Ebola kimenakiliwa nchini Kenya, huku serikali ikiimarisha mikakati ya kukabiliana na uwezekano wa chamko la ugonjwa huo.

Duale alisema kuwa, licha ya Kenya kuwa kitovu cha usafiri katika kanda hii, Wizara ya Afya imeimarisha ukaguzi wa wasafiri katika viwanja vya ndege na mipakani, kuimarisha ufuatiliaji na uwezo wa kuchukua hatua za haraka, imepanua huduma za upimaji katika maabara na kuandaa vituo vya kutenga na kutibu wagonjwa kote nchini.

“Kutokana na chamko za hapo awali, mataifa ambayo yanajitayarisha mapema, hufanikiwa kuokoa maisha, kulinda mifumo yake ya afya na hupunguza kutatizwa kwa chumi zao,” alisema Duale.

Aliongeza kuwa wahudumu wa afya wamepewa mafunzo, vifaa muhimu vya matibabu vimehifadhiwa na kampeni za kuelimisha umma zimeongezwa ili kuhakikisha nchi hii iko tayari kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa kuanzishwa kwa vituo vya karantini na kutenga wagonjwa ni hatua ya tahadhari pekee na si ishara kwamba kuna kisa cha Ebola nchini.

Share This Article