Kiwango cha hatari ya afya ya umma kutokana na mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), kimeongezeka zaidi.
Katika taarifa mpya iliyotolewa Ijumaa, mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema hatari katika eneo pana barani Afrika ilikuwa juu , lakini imesalia ni ya chini katika sehemu zingine za dunia.
Aina adimu ya Ebola, inayojulikana kama Bundibugyo, haina chanjo iliyothibitishwa na inaua takriban theluthi moja ya walioambukizwa.
Hadi sasa, mlipuko huo unaojikita katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo umesababisha vifo takriban 177 na visa vinavyoshukiwa 750.
Hii inakuja huku wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza wakitengeneza chanjo mpya ambayo inaweza kuwa tayari kwa majaribio ya kimatibabu ndani ya miezi miwili hadi mitatu.
Kulingana na teknolojia ile ile waliyotengeneza kwa ajili ya chanjo ya Covid ya AstraZeneca, hakuna uhakika kwamba itafanya kazi na itahitaji utafiti wa wanyama na majaribio kwa watu ili kujua kama itafanya kazi.