Wito wa umoja watolewa kutokomeza ufisadi barani Afrika

Martin Mwanje
2 Min Read
Abdi Mohamud - Mkurugenzi Mtendaji wa EACC

Mamlaka za kupambana na ufisadi barani Afrika zimetakiwa kujibidiisha zaidi na kutumia teknolojia za kisasa kuangamiza jinamizi hilo barani humo. 

Kwa miongo kadhaa sasa, ufisadi umetajwa kuwa kikwazo kikubwa kwa juhudi za kuongeza kasi ya maendeleo barani Afrika.

“Naamini kuwa sisi ndio tumaini la Afrika katika kupambana na ufisadi. Maudhui ya kuimarisha ushirikiano na ubunifu kwa ajili za jitihada zifaazo za kupambana na ufisadi ni azimio letu la pamoja kwamba hakuna asasi hata moja inaweza kukabiliana na tatizo hili peke yake; tunahitaji kufanya kazi pamoja,” amehimiza mwenyekiti wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini Kenya, EACC Dkt. David Oginde.

“Tunahitaji kuimarisha uwezo wa asasi zetu kwa kukumbatia ubunifu. Mfumo wa dijitali unakuwa mgumu zaidi kufanya kazi nao, kwa kutumia mifumo ya awali. Lazima tuwe wabunifu na kutumia akili unde, AI, block chain na teknolojia zingine za kisasa zinazoweza kutumiwa kudhibiti uhamishaji wa rasilimali haraka zaidi.”

Dkt. Oginde aliyasema hayo wakati wa Kongamano Kuu la 8 la kila mwaka la Mamlaka za Kupambana na Ufisadi (AAACA) linalofanyika jijini Nairobi na kuleta pamoja wajumbe zaidi ya 150 kutoka nchi za bara la Afrika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa EACC Abdi Mohamud alielezea matarajio walio nayo  wananchi kwa mamlaka za kupambana ufisadi kusaidia kuangamiza zimwi hilo.

“Wananchi wanatarajia mamlaka za kupambana na ufisadi kuonyesha matokeo dhahiri kupitia ufuatiliaji, kushikilia, kunasa na kurejesha mali zilizopatikana kupitia uhalifu na ufisadi,” alisema Mohamud wakati wa ufunguzi rasmi wa kongamabo hilo la siku tatu lililoanza hapo jana.

“Kushirikishana tajiriba na mbinu bora katika nyanja hii kutaimarisha uwezo wetu wa pamoja wa kuhakikisha mali na rasilimali za umma zilizoibwa zinarejeshwa kwa manufaa ya watu wetu.”

Share This Article