Rais William Ruto amesema Kenya inaunga mkono juhudi za kumaliza vita kati ya Urusi na Ukraine kupitia mazungumzo, diplomasia na kwa kuzingatia sera za Umoja wa Mataifa.
“Tunaamini kuwa amani ya kudumu itapatikana kupitia ushirikiano, uzingatiaji wa sheria za kimataifa na mfumo thabiti wa uwakilishi wa kimataifa,” alisema Rais Ruto.
Aliyasema hayo aliposhiriki mazungumzo na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy pembezoni mwa mkutano wa viongozi wakuu wa Kundi la Nchi Saba zilizostawi zaidi kiviwanda duniani, G7 jijini Évian, Ufaransa.
“Tuliangazia hatua zilizopigwa kwenye uhusiano kati ya Kenya na Ukraine, na kuangazia fursa zilizopo ili kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, kilimo na utoshelevu wa chakula,” alidokeza Ruto.
Anasema walikubaliana kuharakisha mipango ya kubuniwa kwa kituo cha nafaka katika bandari ya Mombasa ili kuimarisha utoshelevu wa chakula na kushughulikia usambazaji Afrika Mashariki.